Sunday, July 7, 2013

MALI YAONDOA HALI YA HATARI


 

Mali imeondowa hali ya hatari Jumamosi(06.07.2013) iliokuwa imedumishwa kwa miezi sita nchini humo ili kuruhusu kuanza kwa kampeni ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 28 mwezi wa Julai. 

Agizo la kuweka muda maalum kwa watu kutoka nje na kupiga marufuku mikusanyiko ya watu lilianza kutumika tarehe 12 Januari siku moja baada ya Ufaransa kufanya shambulio la ghafla la kijeshi kulisaidia jeshi dhaifu la Mali kuwatimuwa wapiganaji wa itikadi kali za Kiislamu waliokuwa wamelidhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo kwa miezi tisa.

Hatua hiyo ya mkoloni wa zamani wa Mali ilikuja wakati wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda wenye kushikilia miji muhimu ya kaskazani walipokuwa wanasonga mbele kuelekea katika mji mkuu wa Bamako.

Mali ilikuja kutumbukia kwenye mzozo wa kisiasa baada ya mapinduzi ya mwezi wa Machi 2012 yaliofanywa na wanajeshi waliokuwa wamekasirishwa kutokana na kutimuliwa kwao kutoka maeneo ya kaskazini na makundi ya waasi ambapo walimlaumu Rais Amadou Toumani waliyempinduwa kwa kushindwa kwao.

Kuondolewa kwa hali hiyo ya hatari kunakuja baada ya jeshi la Mali hapo Ijumaa kuingia kwa amani katika mji wa mwisho uliokuwa ukishikiliwa na waasi.
Wakiandamana na wanajeshi wa Ufaransa na maafisa wa Umoja wa Mataifa, wanajeshi na wanamgambo 200 wa Mali waliingia katika mji wa Kidal ulioko mbali kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

CHANZO: DW

No comments:

Post a Comment